Jeshi
la polisi wilayani Nzega mkoani Tabora jana limemkamata mbunge wa
jimbo la Nzega Dkt. Hamis Kigwangalla aliyekuwa kwenye maandamano ya
wachimbaji wadogo wa dhahabu ya kupinga kufungwa kwa machimbo yao ya
Mwashina yaliyo jirani na mgodi wa Resolute Tanzania Limited.
Kabla ya hapo mbunge huyo alifanya mkutano mkubwa wa hadhara na
wachimbaji hao katika kijiji cha Nzega Ndogo wilayani humo ambapo
alielezwa matatizo ya kufungwa kwa machimbo hayo na kamishna wa madini
nchini Bw. Paulo masanja bila kujali gharama walizoingia wachimbaji hao
wadogo kwenye eneo hilo.
Katika mkutano huo wachimbaji hao walidai ni vema serikali iangalie haki
zao zilizotumika kwenye uendeshaji na uchimbaji wa mashimo hayo kuliko
kuwafungia bila kujali ingawa eneo hilo liko ndani ya leseni ya mgodi wa
Resolute lakini wao ndiyo wamiliki wa ardhi hiyo.
Hata hivyo katika hoja hiyo mbunge huyo aliwataka wachimbaji hao kudai
haki yao kwa kufuata taratibu zinazostahili bila kujali tofauti zao
kisiasa, kikabila na kidini na badala yake wawe kitu kimoja.
Baada ya kauli hiyo mbunge huyo aliwaambia wachimbaji hao wadogo kuwa
haki yao iko mikononi mwao hivyo ni uamuzi wao wa kudai haki yao na yeye
kama mwakilishi wao yuko nyuma yao mpaka pale haki yao itakapopatikana.
Wachimbaji hao walimwomba mbunge huyo kuambatana nao kwenye maandamano
ya amani kutoka kijiji cha Nzega Ndogo kwenda Mwashina yalipo machimbo
yaliyofukiwa umbali wa zaidi ya kilomita tatu kujionea hali halisi ya
kufukiwa kwa eneo hilo na ikiwezekana kufanya mkutano mwingine wa
hadhara kijijini hapo.
Kufuata hali hiyo wachimbaji hao walianza maandamano ambayo yaliungwa
mkono na mbunge huyo hadi kijiji cha Mkwajuni kabla ya kufika Mwashina
ambapo polisi waliibuka na kuyasambaratisha maandamano hayo kwa mabomu
ya machozi na risasi za moto.
Katika na purukushani hizo polisi walifanikiwa kumkamata mbunge huyo na
kumjeruhi mtu mmoja kwa risasi ya moto kwenye paji la uso ambapo
waliondoka nae kwenye gari pamoja na mbunge huyo.
Awali askari wa jeshi hilo waliziba njia na kuwazuia waandishi wa habari
kufanya kazi zao kwa vitisho mbalimbali na matumisi ingawa hali hiyo
ilitulia baada ya maandamano ya wachimbaji kujitokeza.
Kamanda wa polisi mkoani Tabora Suzan Kaganda alipopigiwa simu na
waandishi wa habari alisema hana taarifa yoyote kuhusiana na maandamano
hayo, kukamatwa kwa mbunge huyo wa jimbo la Nzega na kutumika kwa risasi
za moto na mabomu ya machozi kuzuia maandamano hayo.
Tayari Dkt Kigwangala ametoka polisi
Maandamano baada ya mkutano wa Dkt Kigwangala kuelekea eneo la machimbo ya Mwashina wilayani NZega. |
Mlipuko wa mabomu kwa mbali |
Pichani ni mmoja kati ya waandamanaji hao aliyekuwa karibu na Dkt Kigwangala akiwa chini baada ya kujeruhiwa na polisi |
Polisi wakikabiliana na wachimbaji wadogo wa madini wilayaniNzega |
No comments:
Post a Comment