Polisi wametumia gesi ya kutoa machozi, kuwatawanya
vijana wenye hasira waliojaribu kuziba barabara muhimu mjini Mandera,
Kaskazini mwa Kenya , kupinga mauaji ya wahubiri wawili wa kiisilamu
Jumapili usiku.
Waandamanaji waliwasha moto katika barabara
zenye shughuli nyingi mjini humo huku pakiwepo mchezo wa Paka na Panya
kati ya vijana hao na polisi.Wakazi wa mji huo, wametuhumu serikali kwa kuwaua wahubiri wawili nje ya msikiti.
Madai ambayo kamishna mkuu wa mji huo ameyakanusha akisema kuwa wahubiri hao walikuwa sehemu ya genge la watu watatu waliokuwa wanarejea kutoka nchini Somalia, ambako walikuwa wameenda kumsaidia mpiganaji mmoja wa Al shabaab kuingia nchini Kenya.
Inadaiwa kuwa pia walikuwa wameenda kuchukua silaha usiku wa manane.
Kwa mujibu wa duru za usalama, wawili hao wanajulikana sana na waliwahi kuwashambulia polisi kwa maguruneti walipojaribu kusimamisha gari lao kwa ukaguzi.
Polisi wanasema kuwa walifanikiwa kupata maguruneti 8 kutoka kwa gari la washukiwa hao.
Kwa sasa polisi wanamsaka mshukiwa wa tatu ambaye wanasema alikuwa anajaribu kuingia nchini Kenya kimagendo. ambapo inadaiwa alitoroka wakati wa tukio hilo.
Hali ya wasiwasi imeendelea kutanda mjini humo. huku Polisi na wanajeshi wakishika doria katika mji huo unaopakana na Somalia na ambao pia umeshuhudia mapigano ya kikabila nchini humo.
Hivi karibuni watu 16 waliuawa wakati watu wa jamii mbili walipopigania rasilimali na wiki mbili zilizopita polisi wa Kenya waliuawa mpakani mwa Kenya na Somalia huku
Al shabaab wakikiri kufanya mashambulizi hayo.
Kenya imeshuhudia visa kadhaa vya mashambulizi tangu mwaka 2011 wakati wanajeshi wake walipoingia kupambana na Al Shabaab.

No comments:
Post a Comment