WAKATI Watanzania wakisubiri
hatima ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye
Rais Jakaya Kikwete alisema anamuweka kiporo kutokana na kashfa ya
uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge,
ametangaza rasmi kuachia nafasi hiyo.
Bunge
lililopita baada ya kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu mihamala iliyofanyika kwenye Akaunti ya
Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania, lilipitisha
maazimio manane ikiwa ni pamoja na kuazimia kuwajibishwa viongozi wa
Serikali na wale wa kamati za Bunge walioonekana kuhusika katika kashfa
hiyo.
Viongozi wa kamati ambao Bunge liliazimia wawajibishwe ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye pia
ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Victor
Mwambalaswa.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo tulizipata jana, Chenge alitangaza
kujiuzulu nafasi yake juzi baada ya kamati yake kukutana kwenye ofisi
ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.
“Amejiuzulu jana (juzi), saa tano asubuhi wakati wa kikao cha Kamati
ya Bajeti kilichokutana kwenye Ukumbi wa Mkwawa, ofisi ndogo za Bunge
Dar es Salaam.
“Aliwaambia wajumbe kuwa hataki malumbano na wabunge na hataki
msuguano wowote, nafasi yake kwa sasa inashikiliwa na Dk. Festus Limbu,
ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa kamati,” alisema mmoja wa wajumbe wa
kamati hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel, alipotakiwa
kuthibitisha suala hilo, alisema hayuko ofisini, hivyo hawezi kuwa na
jibu la moja kwa moja juu ya suala hilo.
Alisema kama Chenge mwenyewe amefikia uamuzi huo, atakuwa amempunguzia kazi Spika.
Joel alisema kujiuzulu kwake kutakuwa ni kutimiza maazimio ya Bunge jambo ambalo ni lazima litekelezwe.
Akifafanua juu ya kumpata mwenyekiti mpya wa kamati hiyo, Joel
alisema mara baada ya wajumbe hao kukutana kama viongozi hawapo, jambo
la kwanza ni kufanya uchaguzi.
Alisema Chenge alichaguliwa na Spika kuongoza kamati hiyo kwa kuwa ilikuwa ni kamati mpya na ambayo ni nyeti sana.
“Wajumbe wake ukiangalia wengi walitoka kwenye Kamati ya Kushauri
Vyanzo Vipya vya Mapato, Spika aliomba kumchagua mtu ili apate mtu
makini anayejua vyanzo vya mapato,” alisema.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipoulizwa kama ofisi yake ina
taarifa za kujiuzulu kwa Chenge, alisema yupo jimboni na hana taarifa
hizo ila anachojua suala la kuwajibika kwa wenyeviti waliotajwa kwenye
ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) juu ya
kashfa ya Escrow ni la lazima na halihitaji mtu kuandika barua ya
kujiuzulu.
“Hakuna kuandika barua ya kujiuzulu, yale ni maamuzi ya Bunge,
kinachotakiwa ni kamati kukaa na kuchagua viongozi wengine,” alisema.
Ndugai akizungumza nasi juma lililopita,
alisema kamati ambazo viongozi wake walihusishwa na kashfa ya Tegeta
Escrow, zitakapokutana jukumu la kwanza litakuwa ni kuchagua viongozi
wapya kwani tayari chombo hicho kilishaazimia kuwawajibisha.
Katika kashfa ya Escrow, Chenge anadaiwa kupokea Sh bilioni 1.6,
kutoka kwa James Rugemalira ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya VIP
Engineering iliyokuwa na asilimia 30 kwenye Kampuni ya Independent Power
Tanzania Limited (IPTL), inayodaiwa kuuzwa kinyemela kwa Kampuni ya Pan
African Power (PAP
No comments:
Post a Comment