Friday, 14 August 2015

MAJINA YA WALIOCHAGULIWA KUGOMBEA MAJIMBO CCM, YAMETOLEWA RASMI.

Majina ya walioteuliwa kugombea ubunge wa majimbo na uwakilishi wa viti maalum kupitia CCM katika majimbo yote Tanzania yametoka rasmi , yupo Iddi Azzan anagombea Jimbo la Kinondoni, Prof. Anna Tibaijuka anagombea jimbo la Muleba Kusini.

Nape Nnauye anagombea jimbo la Mtama., Nimrod Mkono anagombea jimbo la Butiama, Ndugu Ridhiwani Kikwete anagombea Chalinze na Job Ndugai ameteuliwa kugombea Kongwa.


Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Jana ilitangaza majina ya wagombea ubunge, ubunge viti maalum, uwakilishi na uwakilishi viti maalum ambapo baadhi ya wagombea walioshinda kwenye kura za maoni wametupwa nje na kuchukuliwa mshindi wa tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya CCM mjini Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi Bw,Nape Nnauye amesema kuwa kuna baadhi ya majimbo ambayo yamelazimika kurudia kupiga kura za maoni na mengine kuhesabu upya kura zilizopigwa baada ya kujitokeza malalamiko kwa wagombea.
Amesema kuna baadhi ya majimbo ambayo wamelazimika kumchukua mshindi wa tatu kwenye kura za maoni na kuwaacha walioshinda nafasi ya kwanza na ya pili ili kumaliza migogoro iliyokuwepo.
Ameyataja majimbo 11 ambayo yatarudia uchaguzi wa kura za maoni kuwa ni Ukonga, Kiteto, Chilonwa, Kilolo, Njombe Kusini, Makete, Namtumbo, Rufiji, Mbinga Vijijini, Busega na Singida Mashariki.
Aidha Nnauye amesema kuwa uchaguzi wa viti maalum kupitia umoja wa wanawake Tanzania (UWT) yamepitishwa kama yalivyotoka mikoani ambapo ni mkoa mmoja tu wa Dar es Salaam ambao NEC imetengua ushindi wa mshindi wa kwanza, Angela Kiziga ambaye ni mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na badala yake aliyeshika nafasi ya pili na ya tatu ndiyo waliopitishwa katika ubunge wa viti maalum.
Waliopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM kwenye ubunge wa viti maalum mkoa wa Dar es Salaam ni Mariam Kisangi aliyekuwa mshindi wa pili na Janeth Masaburi aliyekuwa mshindi wa tatu.

No comments: