![]() |
Ali Kiba na Diamond |
Ikiwa imebaki
siku moja kabla ya uchaguzi mkuu, hatimaye mgombea wa nafasi ya urais
kwa leseni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli
amemaliza yale mabifu sugu kati ya manguli wawili wa Bongo Fleva, Ali
Saleh Kiba na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na lile la Wema Isaac
Sepetu na Aunt Ezekiel, Ijumaa linaweza kuripoti.
KIBA NA DIAMOND
Uchunguzi wa gazeti hili ambalo
limeambatana na Magufuli takriban mikoa yote ya Tanzania kwenye kampeni
zake umeonesha wazi kuwa kwa sasa Kiba na Diamond wamezika tofauti zao.
Katika kuzunguka sehemu mbalimbali
mikoani kwa ajili ya Magufuli, jamaa hao walikutana mara kadhaa na
kuchangamkiana huku watu wakiwatania na kujikuta wakiishia kucheka.
KOLABO YA KIBA NA DIAMOND
Kwa mujibu wa Team Magufuli,
watahakikisha wawili hao wanafanya kolabo hivi karibuni mara tu baada ya
pilikapilika za uchaguzi kumalizika.
“Unajua mheshimiwa amefanikiwa
kuwakutanisha mara nyingi sehemu mbalimbali mikoani na wote amezungumza
nao juu ya kutaka kuwaona wakifanya kazi pamoja.
“Alichowasisitizia mheshimiwa ni kuona
wasanii wanakuwa na umoja na kwamba atawaunganisha wote bila kujali
tofauti zao ilimradi wawe kitu kimoja.
![]() |
Mh,John Pombe Magufuli. |
SASA MAMBO FRESHI
“Mheshimiwa yeye hajali wasanii wa CCM
pekee, amesema hata wale wa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi)
atawasaidia bila kujali itikadi ya vyama hata kama hawakumuunga mkono,”
alisema mmoja wa Team Magufuli anayeshughulika na ratiba za wasanii
kwenye kampeni na kuongeza:
“Hata wakati wa kusaini mikataba ya shoo
walikuwa wanakutana mara kwa mara na kupeana tano kuonesha kwamba sasa
mambo ya bifu yamekwisha.”
MSIKIE KIBA
Akizungumzia bifu lake la muda mrefu na Diamond, Kiba alifunguka: “Mimi sioni faida ya mabifu na mashabiki ndiyo wanakua mambo.”
HUYU HAPA DIAMOND
Kwa upande wake Diamond aliliambia Ijumaa
kuwa, kwa sasa hana bifu lolote na jamaa huyo na kwamba mheshimiwa
amewasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuufikisha muziki wa
Bongo Fleva mbali na ikiwezekana duniani kote.
“Mheshimiwa ameahidi kutupiga tafu ili
muziki wetu ufike mbali zaidi. Hayo mambo ya bifu yameshapitwa na
wakati, sasa hivi ni kazi tu,” alisema Diamond.
MAKUNDI MITANDAO YA KIJAMII
Kufuatia hali iliyopo kwa sasa, hata
yale makundi hasimu ya Team Kiba na Team Diamond yanaonekana kujirudi na
kuwa kitu kimoja hasa lilipokuja suala la kumsapoti Magufuli ambapo
imekuwa ni rahisi kwa kundi moja kuliunga mkono kundi lingine kwenye
mitandao ya kijamii ya Instagram, WhatsApp, Facebook na Twitter.
BIFU TANGU 2012
Kabla ya kumaliza tofauti zao, Kiba na
Diamond wamekuwa kwenye bifu zito tangu mwaka 2012 ikielezwa ni
ushindani katika muziki wao ambapo kila mmoja alikuwa akijiona yupo juu
kuliko mwingine.
![]() |
Wema Sepetu |
WEMA NA AUNT
Kwa upande wao, mashosti wawili ambao
walikuwa wameshibana vilivyo kisha kuhitilafiana, Wema na Aunt, nao
wamejikuta wakimaliza tofauti zao, kisa kumpigia kampeni Magufuli.
KISA DIAMOND
Awali, Aunt na Wema walikuwa hawaivi
baada ya Aunt kuwa upande wa Diamond katika kipindi ambacho Wema alikuwa
haivi na jamaa huyo ambaye alikuwa mwandani wake kabla ya kunasa kwenye
penzi la mwanamama Zarinah Hassani ‘Zari The Boss Lady’.
Pia wakati kampeni zinaanza, Aunt
alikuwa upande wa Ukawa, akiwa ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) akimuunga mkono Edward Lowassa hivyo bifu lake na
Wema lilikuwa kama ndiyo limechochewa moto.
AUNT KUREJEA CCM
Lakini Aunt aliporejea CCM na kutangaza
kumsapoti Magufuli ndipo Wema naye akarejesha urafiki wake na mwanadada
huyo kwa msaada wa Team Magufuli.
Pamoja na kwamba kila mmoja alikuwa
kitengo chake cha kampeni ambapo Wema alikuwa kwenye Kampeni ya Mama
Ongea na Mwanao huku Aunt akiwa Nimestuka lakini bado walikuwa
wakionesha ukaribu na ushosti wao kupitia mitandao ya kijamii.
AUNT ANASEMAJE?
Kuhusu kupatana na Wema, Aunt alifunguka: “Mambo ya bifu tupa kule hapa ni kazi tu!”
WEMA VIPI?
“Sina bifu na Aunt. Kwa sasa tunaweka nguvu zote kwenye ushindi wa Magufuli,” alisema Wema kwa kifupi.
WEMA NA DIAMOND
Duru za habari zilieleza kwamba ni
kampeni hizihizi za Magufuli ambazo zimefanikisha kumaliza bifu la Wema
na Diamond lililodumu kitambo tangu walipoachana mapema mwaka jana.
WEMA, DIAMOND URAFIKI UPYA
Wawili hao walifufua urafiki wao mapema
wakati wa ufunguzi wa Kampeni za Magufuli kwenye Viwanja vya Jangwani
jijini Dar ambapo inadaiwa walikutana nyuma ya jukwaa (back stage) na
kuchangamkiana kisha kumaliza bifu lao na sasa kila wanapoonana ni
kicheko tu.
Haikuwa kazi rahisi
Mmoja wa wadau wa muziki aliyekuwa
kwenye kampeni za Magufuli anayedili na mastaa ambaye hakupenda jina
lake liandikwe gazetini alisema: “Haikuwa rahisi kuwapatanisha mastaa
hao ambao kila mmoja alikuwa akimpiga vita mwenzake na wanaomunga
mkono.”
No comments:
Post a Comment