Monday, 23 November 2015

RAIS J.P.MAGUFULI AFUTA MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU.{9th DECEMBER}

Rais John P. Magufuli amefuta maadhimisho ya siku ya Uhuru tarehe 9 Disemba mwaka huu, siku hiyo itatumika kwa ajili ya kufanya usafi nchi nzima kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu

-Ameagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa shughuli hiyo zikafanyie shughuli nyingine.....


=======================================================================

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425


OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kwa mujibu wa Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike kwa kufanya kazi. Kwamba maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu. Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.

Aidha, kwa kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.

Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo, sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
23 Novemba, 2015

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiongea na waandishi wa habari

 Kauli ya Katibu Mkuu Kiongozi kwa niaba ya Rais Magufuli

"Rais amesema suala la kuwepo ugonjwa Kipindupindu halikubaliki, jambo hili limemkera sana, tunasherehekea miaka 54 ya uhuru lakini bado kipindupindu kinatusumbua sana. Amesema kama Watanzania lazima tulishughulikie. Haiwezekani akija mgeni kama Obama tunafanya usafi lakini akiondoka tunaendelea kuwa wachafu. Ameamua tarehe 9 December siku ya Uhuru hakutakuwa na sherehe yoyote badala yake watu wakasafishe maeneo yao”

"Amesema hakutakuwa na cha kwenda kwenye Gwaride, kila mkuu wa Mkoa au kiongozi yeyote wa eneo husika wanatakiwa waanze kuandaa vifaa vya usafi, itakuwa ni siku ya kufanya usafi ili kupunguza tatizo la uchafu..

Si kwamba tuna dharau siku hii bali tunaifanya kwa staili nyingine… Kuhusu pesa zitakazotumika siku hiyo Rais atatafuta kazi ya kuzifanyia, atazipeleka kwenye eneo lingine lenye tatizo"

No comments: