Friday, 6 November 2015

Rais Magufuli amuapisha Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju akila kiapo Ikulu Jijini Dar es Salaam mbele ya Rais John Magufuli
RAIS wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amemuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju asubuhi ya leo Novemba 6, 2015, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kuapishwa kwa mwanasheria huyo kunakuja ndani ya saa 24 baada ya Dk. Magufuli kuapishwa jana Novemba 5, 2015 kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano, ambapo hapo jana muda mfupi baada ya kukabidhiwa madaraka kama Rais wa nchi aliweza kumteua Masaju kushika nafasi hiyo.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kwa waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, ilieleza kuwa Rais Magufuli atamuapisha mwanasheria huyo leo asubuhi ili kuanza majukumu yake mara moja kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Rais Magufuli ameitisha rasmi kikao cha kwanza cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kitakachoketi Novemba 17, mwaka huu, Dodoma.
Katibu Mkuu Kiongozi alikaririwa akisema pia kuwa Rais Magufuli anatarajiwa kupendekeza jina la Waziri Mkuu ambalo litawasilishwa katika Bunge hilo jipya Novemba 19 ili lipigiwe kura.
Kabla ya uteuzi wake, Masaju alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali mnamo mwaka 2009, aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu baada ya aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo Jaji Fredrick Werema kujiuzulu nafasi yake. 
Jaji Werema alijiuzulu nafasi hiyo Desemba 2014 kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow kwa madai kuwa ushauri wake alioutoa kuhusu suala hilo haukueleweka na badala yake alichafua hali ya hewa na hivyo alikana kuhusika moja kwa moja katika kashfa hiyo .
Hata hivyo, hadi sasa anafanyakazi kama Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sheria Tanzania ambapo pia amepata kuwa Mshauri wa Sheria wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika serikali ya awamu ya nne.

No comments: