Friday, 18 December 2015

Tanzania kuanzisha mazungumzo ya kusuluhisha mgogoro wa Burundi.

Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Mambo ya nje Dkt. Agustine Mahiga, kuanzisha mazungumzo ya kusuluhisha mgogoro wa kisiasa wa Burundi.

-Waziri Mahiga amesema kuwa ufumbuzi wa kisiasa pekee na sio mtutu wa bunduki utamaliza mgogoro Burundi.


Wakati wakimbizi kutoka Burundi wakiendelea kumiminika kambini mkoani Kigoma, Rais Magufuli amemuagiza waziri wa mambo ya nje, ushirikiano wa kimataifa, Afrika Mashariki na Kikanda, Dr Augustine Mahiga, kufufua maongezi ya Amani na mawaziri wenzake wa Afrika Mashariki wanaoshughulikia uhusiano wa kimataifa kuhusu mgogoro unaoendelea Burundi.

Habari kutoka Wizara ya Mambo ya ndani zinasema kufikia sasa Zaidi ya Warundi 120,000 wamekimbia makazi yao na kuingia Tanzania.

Dr Mahiga amesema tayari ameanza kuzungumza na Mawaziri wenzake ili kupanga mikakati ya jinsi watakavyoendesha mazungumzo hayo muhimu, kama alivyoagizwa na mkuu wake Dr Magufuli.

Dr Mahiga amesema kuwa ufumbuzi wa kisiasa pekee na sio mtutu wa bunduki, utamaliza mgogoro nchini Burundi. Amesisitiza kuwa wanatafuta Amani kwa maongezi ya pande mbili.

Wengine atakaokutana nao katika kukamilisha jukumu lake ni pamoja na katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dr Richard Sezibera ambaye atakwenda kuzungumza naye Arusha.

Waziri Mahiga pia amesema Umoja wa Mataifa unashughulikia jambo hili kwa ukaribu na ameshazungumza na Balozi wa Marekani nchini juu ya hali ya kisiasa nchini Burundi.

Wakati hayo yakiendelea, mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR-RCS) kupitia mwenyekiti wake Joseph Butiku, nao umeonyesha nia ya kutaka kuwa sehemu ya ufumbuzi wa tatizo la Burundi. Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam wakati wa kumalizia mkutano wa siku mbili uliokuwa na dhumuni la kujadili utatuzi wa matatizo mbalimbali ya kanda ya Afrika Mashariki.

============================== ========
My Take
Mgogoro wa Burundi, mtihani wa kwanza wa Magufuli kimataifa


Wanabodi,

Wakati watu wengi wakisifia utendaji wa mheshimiwa Rais hadi kwenye mtandao wa kijamii kuanzishwa 'hashtag' #WhatWouldMagufuliDo , macho na masikio yanaelekezwa kwake. Tanzania ikiwa ndio mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sasa Rais wetu hana budi kutumia nafasi yake kuwa sehemu muhimu ya utatuzi wa mgogoro huu.

Hadi sasa ameshatoa maagizo kwa Waziri anayehusika na mahusiano ya kikanda Augustine Mahiga kukutana na wenzake wa nchi za maziwa makuu kutafuta suluhu.

Tukumbuke nchi yetu ina rekodi nzuri ya usuluhishi wa migogoro ya aina hii kuanzia kwa Nyerere hadi Jakaya Kikwete aliyepita, naamini kauli ya Rais ina uzito mkubwa na wengi watakuwa wanasubiri kusikia msimamo wetu kama taifa.
 

No comments: