JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia mganga
wa kienyeji, Simba Said (44) mkazi wa Vingunguti Koloni, Dar es Salaam
kwa tuhuma za kuwafanyia dawa majambazi kabla ya kwenda kufanya matukio
ya uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Simon Sirro, alisema taarifa
za kuwapo kwa mganga huyo walizipata kutoka kwa raia mwema.
Alisema baada ya kumkamata na kumhoji, alikiri kuwafanyia dawa watu wanaodaiwa kuwa majambazi.
“Mganga huyo aliyekamatwa eneo la Buguruni, alikiri kuwafanyia dawa
majambazi ili wasikamatwe. Anasema amewafanyia dawa wengine ambao
walikuwa wamejipanga kwenda kufanya uhalifu eneo la Buguruni,” alisema.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, waliweka mtego, lakini walipotaka kuwakamata majambazi hao walishtuka.
Kamanda Sirro alisema polisi walilazimika kuwarushia risasi na
kufanikiwa kumjeruhi jambazi mmoja ambaye alipelekwa Hospitali ya Amana
kwa ajili ya matibabu, lakini alifariki dunia.
Alisema majambazi wengine walifanikiwa kukimbilia eneo la Tabata wakitumia pikipiki tatu.
Aliwataja watuhumiwa hao ni Ibrahimu Mussa (40) mkazi wa Mbagala,
Mohamedi Shaibu (20) mkazi wa Magomeni, Khamisi Jafari (44) mkazi wa
Makambako na Abdulaziz Kikwanda (44) ambaye ni mlinzi na mkazi wa
Buguruni.
“Wengine ni Juma Bakari (40) mkazi wa Majohe, Fitina Ramadhani (43)
mkazi wa Magomeni Kagera, Dunia Rashid (50) mkazi wa Magomeni na Khamis
Omary (36) Buguruni,” alisema Kamanda Sirro.
Wakati huo huo, jeshi hilo linamshikilia jambazi sugu Mkama Maiga
(32) mkazi wa Mbagala Majimatitu aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu.
Kamanda Sirro alisema mtuhumiwa huyo alipopekuliwa katika nyumba
yake, alikutwa na bunduki aina ya Chinese ikiwa imefutwa namba zake.
No comments:
Post a Comment