Friday, 21 February 2014

MWANAMKE MWENYE NDEVU NYINGI KAMA MWANAUME APATA VITISHO VYA KUUAWA..

Harnaam Kaur, mwanamke mwenye umri wa miaka 23 anayeishi katika mji wa Slough, Kusini Mashariki mwa Uingereza amepokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu asiowafahamu kwenye mitandao kwa sababu ya ndevu zake nyingi zinazomfanya asitofautishwe kirahisi na mwanaume. Mwanamke huyo ambaye anakabiliwa na tatizo la kuwa na vinyweleo vingi kupita kiasi mwilini mwake, tatizo linalojulikana kitaalamu kama ‘polycystic ovary syndrome’, ameeleza kuwa alianza kupata tatizo hilo akiwa na umri wa miaka 11 na kwamba alikuwa akizinyoa mara mbili kwa wiki. Ameeleza kuwa alipokuwa shuleni alikuwa akionewa sana kwa kuitwa majina mengi ya kejeli kama ‘jike dume’, na kwamba alikuwa anashindwa hata kuwaangalia watu usoni na alipotoka shule alijifungia ndani siku zote asionekane mara kwa mara. Ameongeza kuwa kutokana na kuishi katika hali hiyo alifikia hatua ya kufikiria kutaka kujiua. Hata hivyo, Harnaam amesema kuwa amejiunga na dini ya Sikh na kubatizwa, na kwamba imani ya dini hiyo hairuhusu watu kunyoa vinyweleo vyao kwa ya kuwa Mungu ndiye aliyewaumba hivyo. Kwa hiyo ameziachia nywele zake na sasa anaonekana kama mwanaume akiwa na nywele nyingi kidevuni, mikononi na kifuani. Imani hiyo imempa ujasiri zaidi juu ya muonekano wake, na anajiona mwanamke mwenye mvuto zaidi. “Nahisi nimekuwa mwanamke zaidi, nina mvuto zaidi na nadhani naonekana hivyo pia. Nimejifunza kupenda jinsi nilivyo na hakuna kitakachonitikisa sasa hivi.” Amesema Harnaam.
“naweza kwenda kwenye maduka ya wanawake bila kuhisi kuwa sitakiwi kuwa kule. Navaa skirts, gauni na vidani na napenda kutengeneza kucha zangu kama msichana mwingine yeyote.”alisema Hamaam Kaur.

No comments: