Wednesday, 19 March 2014

WAZIRI MAHAKAMANI KWA UFISADI-KENYA.

Waziri wa zamani wa ardhi Amos Kimunya
Waziri wa zamani katika serikali nchini Kenya, Amos Kimunya amefikishwa mahakamani mjini Nairobi kwa makosa ya kutumia vibaya mamlaka pamoja na kujipatia ardhi ya umma kinyume na sheria.
Waziri huyo wa zamani wa Ardhi, aliwasili mahakamani hapo jana kujibu mashitaka hayo.
 Bwana Kimunya pamoja na washitakiwa wenzake ambao ni pamoja na afisa mmoja wa ardhi na afisa wa kampuni inayomilikiwa na Kimunya, kwa pamoja walifikishwa katika mahakama maalum nchini humo ya kupambana na ufisadi kujibu mashitaka saba ya utumiaji mbaya wa mamlaka na kujipatia ardhi kwa njia ya udanganyifu.

Mwendesha mashitaka mkuu wa  Keriako Tobiko, anadai kuwa bwana Kimunya alipokuwa waziri wa ardhi, akishirikiana na afisa mmoja wa ardhi walitumia mbinu ya udanganyifu kujipatia kampuni moja inayomilikiwa na Kimunya , ardhi yenye thamani ya shilingi milioni sitini.
Kimunya pia alifahamishwa na mahakama kuwa alifanya kitendo hicho bila ya kujulisha serikali kuwa alikuwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo.
Vile vile alishitakiwa kwa kosa la kukosa kulinda ardhi ya umma.
Kimunya na washitakiwa wenzake wamekanusha mashitaka dhidi yao.
Awali alipokuwa waziri chini ya serikali ya Rais wa zamani Bw,Mwai Kibaki, Kimunya  alihusishwa pia na sakata la kuuza moja ya hoteli za kifahari nchini Kenya Grand Regency kwa kampuni ambayo yeye alikuwa mkurugenzi wake.

No comments: