Jambo limezua jambo zile milioni 13 alizolipa staa mkubwa wa kike hapa
Bongo, Wema Isaac Sepetu aka Beautiful Onyinye mahakamani ili kumnusuru
Kajala Masanja kwenda jela, zinaendelea kusababisha fukuto na sasa
Kajala amejibu mapigo, akisema hatamlipa Wema fedha hizo.
Wema na Kajala wapo kwenye mgogoro mzito kwa muda mrefu huku mashabiki wa
mastaa hao waliojipa majina ya Team Wema (wanaomuunga mkono Wema) na
Team Kajala (walio upande wa Kajala) wakiukuza ugomvi huo kwa
kushambuliana kwa maneno makali kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
WEMA KUFUNGUKA
Katika gazeti moja, toleo namba 877 la Aprili 25-Mei Mosi, 2014 la wiki
iliyopita, liliandika habari ya Wema iliyokuwa na kichwa; Kwa mara ya
kwanza Wema afunguka, asema: NAJUTA KUMLIPIA KAJALA MIL. 13!
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Wema kufunguka baada ya bifu la
kimyakimya la muda mrefu ambapo alifafanua chanzo cha bifu lao na namna
anavyojuta kumlipia Kajala fedha hizo.
“Kusema kweli najuta kumlipia (Kajala) ile faini ya Sh. milioni 13. Bora
angeenda jela miaka saba kuliko kunisababishia matatizo na maumivu
kiasi hiki. Mimi sijawahi kumsema vibaya K kisa eti nilimlipia fedha
hizo,” alisema Wema katika gazeti hilo.
Alipoambiwa kama Kajala yupo tayari kurudisha fedha hizo alisema:
“Kama anataka kunilipa, anilipe kisha aende jela maana mimi sikumkopesha, nilitoa kwa moyo.”
HABARI ZA MOTO
Baada ya gazeti hilo kuruka mitaani na Kajala kulipata ndipo akaeleza mambo mazito.
Akizungumza na mwanahabari, Kajala alisema katika vitu ambavyo Wema
anatakiwa kuvisahau ni pamoja na kumlipia mahakamani hizo milioni 13.
“Siwezi kumlipa ng’o. Namlipa nini sasa na kivipi? Kwani tulikopeshana?
Hakuna anachonidai Wema, hata kama akisema nimlipe, siwezi kufanya
hivyo,” alisema Kajala.
Huku akimwaga machozi, Kajala aliendelea: “Unajua haya mambo
yanachukuliwa kirahisi tu na wadandiaji wa mambo, ni vile watu hawajui
ni kwa kiwango gani hili suala linaniumiza.
“Wema alinisaidia, alinilipia fedha mahakamani wakati ambao nilikuwa na
uhitaji na sikuwa na zile fedha. Kama asingejitokeza kunilipia nilikuwa
nakwenda jela.
“Lile ni jambo kubwa. Thamani yake haifananishiki na fedha. Ule ulikuwa
ni utu tu, sasa leo iweje ligeuzwe kuwa kama deni? Siwezi kufanya
hivyo.”alisisitiza Kajala.


No comments:
Post a Comment