Pichani Kinamama walio karibu na familia ya marehemu Isabela Andrew aliyebakwa
hadi kufa wakiangua kilio baada ya kushuhudia mahali mwili wake
ulipokutwa huko Area C mjini Dodoma jana.
Mfanyakazi wa ndani, Isabella Andrew (18), amefariki dunia na kifo
chake kikidaiwa kusababishwa na kubakwa na watu wasiojulikana.
Mwili wa msichana huyo ulikutwa ukiwa umeharibika katika moja ya pagale,
lililopo Area C, Dodoma Mjini na mwandishi wetu alishuhudia ukitolewa
hapo kwa machela huku polisi wakiwahoji mashuhuda wa tukio hilo.
Mkazi wa Mtaa wa Kiwanja cha Ndege, Jackson Coy aliyekuwa akiishi na
binti huyo alisema msichana huyo alipotea tangu Jumamosi iliyopita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema mwili huo
uliokotwa jana saa mbili asubuhi na kwamba polisi wanaendelea na
uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake.
Mwili huo ulibainika
baada ya mama mmoja, Rehema Msambile kufika katika pagale hilo alipokuwa
akifuatilia nyendo za mtoto wake ambaye juzi alipigwa kwa tabia ya
utoro shuleni.
“Niliamua leo (jana) kumfuatilia, nikaanza
katika mapagale.Nilipofika hapa ndipo nikaona mwili wa marehemu ikabidi
nimuite jirani hapo aje aone,” alisema.
Diwani wa Kata ya
Kiwanja cha Ndege, Henry Kandenga alisema mazingira yanaonyesha kuwa
binti huyo alibakwa kwa sababu walikuta nguo za ndani zikiwa pembeni.
“Hakuna yowe iliyosikika kwamba kuna mtu anauawa ukizingatia kwamba
nyumba ziko jirani na hata nyumba aliyokuwa akiishi ni jirani na mahali
alipokutwa,” alisema .
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma. |
No comments:
Post a Comment