Saturday, 18 October 2014

MEYA MANISPAA YA TABORA NDANI YA KASHFA NZITO YA UFISADI.

Meya wa Manispaa ya Tabora Bw,Gulam Hussein Dewji akiongea na Wanahabari muda mfupi baada ya kutoka kwenye mahojiano na Baraza la maadili ya viongozi ndani ya ukumbi wa karimjee siku ya jana.

Kwa ufupi Ni Meya wa Tabora, anatuhumiwa kushindwa kutangaza mali zake anazozimiliki kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Dar es Salaam Meya wa Manispaa ya Tabora, Gulam Hussein Dewji ameshushiwa tuhuma nzito za kuidanganya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushindwa kutangaza mali anazozimikiki zikiwamo pikipiki 422, licha ya kutakiwa kufanya hivyo kisheria. Sheria Namba 5 ya mwaka 2001 ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inamtaka kila kiongozi kujaza fomu za kutangaza mali zake na madeni na kuziwasilisha kwenye Sekretarieti hiyo kila mwisho wa mwaka. Meya huyo alisomewa mashtaka yake jana na Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus mbele ya Mwenyekiti wa Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisi Msumi. Mwanasheria huyo alisema kuwa meya huyo anatuhumiwa kutotamka baadhi ya mali anazozimiliki na kuzitaja mali hizo kuwa ni pikipiki 422, magari matatu, viwanja vitano na nyumba moja. Cyriacus alisema kwamba meya huyo alishindwa kutangaza mali zake katika kipidi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2010 hadi 2013. Tuhuma nyingine zinazomkabili meya huyo ni kuchukua Sh2.6 milioni mali ya Manispaa ya Tabora kwa ajili ya safari yake kwenda nchini Marekani. “Mwaka 2012 meya huyo alipata mwaliko wa kwenda Marekani ambako waliomwalika walimlipa gharama zote alipofika nchini humo lakini yeye aliomba fedha katika manispaa hiyo kwa maelezo kwamba angezirejesha baada ya kulipwa, lakini hadi sasa hajafanya hivyo,” alisema. Akitoa ushahidi wa tuhuma hizo, Ofisa Maadili wa Sektetarieti hiyo, Gerald Mwaitebele huku akiwasilisha vyaraka kwa Jaji Msumi, alisema kuwa nyaraka kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zinaonyesha kuwa mmiliki wa pikipiki na magari hayo ni Gulam Dewji. “Nawasilisha matamko ya mali ambayo hayaonyeshi pikipiki 422, magari matatu, viwanja vitano na nyumba moja inayomilikiwa na Gulam Hussein Dewji,” alisema. Alisema: “Licha ya mali hizi kumilikiwa na meya, lakini hazionekani kwenye fomu za matangazo ya mali, huu ni udanganyifa mwenyekiti.” Meya Dewji atapata muda wa kutoa utetezi wake katika kikao kijacho cha baraza hilo, baada ya mashahidi watatu kutoa ushahidi wao mbele ya tume hiyo. Jaji Msumi aliahirisha shauri hilo hadi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itakapopanga tarehe nyingine.
Credits-MWANANCHI

No comments: