Monday, 14 September 2015

Amani Karume Achukizwa Na Lugha Za Matusi Kwenye Kampeni Ya CCM

Rais wa serikali ya awamu ya sita ya mapinduzi ya Zanzibar, Amani Abeid Karume
Rais wa serikali ya awamu ya sita ya mapinduzi ya Zanzibar, Amani Abeid Karume ameonyesha kuchukizwa na lugha za matusi zilijitokeza katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea.
Akizungumza leo katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za urais za CCM, muda mfupi baada ya kada mmoja wa chama hicho kumshambulia kwa lugha za kuhudhi mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, Duni Haji Duni, rais huyo wa zamani aliwataka wanasiasa kufanya kampeni za kistaarabu ili kuendelea kuilinda amani na utulivu wa nchi .
Kada huyo wa CCM alimtaja Juma Haji Duni kama ‘bwege, jinga na mbumbumbu’, maneno ambayo ni dhahiri kuwa Amani Abeid Karume hakufurahishwa nayo.
“Hata unapoongea na jirani yako aliyemwaga maji machafu mlangoni kwako, hakuna lugha nyingine ya kumweleza zaidi ya matusi?” Alihoji Amani Karume.
Amani Karume aliwasihi wananchi wa Zanzibar kuhakikisha wanatunza amani iliyopo kwa kuwa ahadi tele zinazotolewa na wagombea kumi na nne wa urais wa Zanzibar hawataweza kuzitekeleza endapo hakutakuwa na amani.
Rais huyo ambaye alitumia zaidi salamu ya kitaifa ya ‘Mapinduzi’, alihitimisha kwa kueleza kuwa yeye huwa hana tabia ya kumuongelea mtu kwa kuwa uamuzi wa kutekeleza hufanywa na mgombea mwenyewe pindi atakapoingia madarakani.

No comments: