Thursday, 22 October 2015

UKAWA WATOA TATHMINI YA UCHAGUZI MKUU 2015.

Mgombea Urais kupitia UKAWA Mh,Edward Lowassa.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai mgombea wake wa urais, Edward Lowassa anayeungwa mkono na Ukawa ataibuka na ushindi wa asilimia 61 katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumapili ijayo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampeni za chama hicho, Reginald Munisi alidai katika tathmini iliyofanyika wiki iliyopita kimebaini kuwa mgombea wake ataibuka na ushindi huo.
“Wiki iliyopita tulifanya tathimini yetu. Kama chama cha siasa ni lazima ufanye jambo hili ili kuona utashinda kwa asilimia ngapi na unakubalika kiasi gani. Tumebaini kuwa tutashinda kwa asilimia 61 na hata ikipungua haitazidi asilimia 58,” alidai Munisi.
Alisema matokeo hayo yalitokana na wananchi 30,000 waliohojiwa katika mikoa yote nchini lakini alikataa kufafanua kwa kina methodolojia wanayotumia kufanya tathimini hiyo kwa sababu ya “kimkakati”.
Alisema Lowassa ambaye atahitimisha kampeni za Chadema na Ukawa kesho kutwa katika viwanja wa Jangwani, Dar es Salaam, anakubalika kwa kiasi kikubwa na wananchi.
Hii ni mara ya pili kwa Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF kutoa matokeo ya utafiti wao. Mara ya kwanza ilikuwa Septemba 24 baada ya mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia kusema utafiti uliofanywa sehemu tatu tofauti ulimpa Lowassa ushindi wa asilimia 71
Vilevile, Chadema kimetaja kasoro zilizopo katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na mfumo wa kujumlisha matokeo na kutoa saa 24 kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa ufafanuzi, ikishindiwa, kitatangaza msimamo wake leo.
Alisema kuna watu wanaofahamu Chadema na Ukawa unaoundwa na NCCR-Mageuzi, NDL na CUF wataibuka na ushindi na kuanza kufanya hila kuhakikisha haupatikani.
“Kuna mambo mengi yanafanyika ikiwamokuwakatisha tamaa wananchi. Tunaitaka NEC na Serikali kuwaacha wananchi wapige kura ili wapate viongozi wanaowataka, kinyume na hapo watazua tafrani kubwa,” alisema.
Alipoulizwa iwapo watayakubali matokeo, alisema: “Tukishindwa kwa haki tutayakubali, lakini kinyume na hapo ni ngumu. Ila hata wao pia wajiandae kisaikolojia iwapo tutashinda na hatutakuwa na kisasi na mtu.”
Munisi alidai taarifa walizonazo zinalenga kufanikisha ‘bao la mkono’ kuwa ni kuvuruga kwa muda mawasiliano ya simu na mitandao siku ya uchaguzi na kuzimwa kwa umeme katika maeneo ambayo Ukawa wana nguvu.


CHANZO: MWANANCHI

No comments: