Thursday, 19 November 2015

VIDEO:-Mwanasheria Mkuu abomoa hoja za UKAWA, Asema hazina mantiki kikatiba!


Mwanasheria nguli nchini ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa serikali, ametumia dakika moja tu kuvunja vunja hoja zote ambazo ziliibuliwa na UKAWA kuhusu uhalali wa rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Shein, kuhudhuria kwenye uzinduzi wa Bunge.
Masaju bila ya kubwabwaja alitumia ibara ya 102 ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ambayo inaeleza kuwa, kutakuwa na serikali ya Zanzibar itakayo julikana kama serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ambayo itakuwa na mamlaka katika Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo mambo ya muungano kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.
Baada ya hiyo, akatumia ibara ya 103 ibara ndogo ya kwanza ya katiba ya jamhuri inasema kuwa, kutakuwa na kiongozi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ambaye ndiye atakuwa rais wa Zanzibar na mkuu wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na vilevile mwenyekiti wa baraza la mapinduzi.
Baada ya Ibara hizo, akajielekeza kwenye katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 katika Ibara yake ya 26 ambayo inasema, kutakuwa na rais wa Zanzibar ambaye atakuwa mkuu wa nchi ya Zanzibar, kiongozi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi.
Hali kadhalika akanukuu Ibara ya 27 ambayo inaeleza namna rais wa Zanzibar atakavyo patikana. Ambayo inasema kwamba, rais atachaguliwa kufuatana na katiba hii na kwa mujibu wa sheria yoyote itakayotungwa na baraza la wawakilishi kuhusu uchaguzi wa rais na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi na uchaguzi wa rais utafanyika katika tarehe itakayowekwa na tume ya uchaguzi (ikiwa na maana ya ZEC).
Aidha, alinukuu Ibara ya 28 (a) ya katiba ya Zanzibar ambayo inaeleza kwamba, kufuatana na katiba hii, mtu ataendelea kuwa rais mpaka: a) Rais anaefata ale kiapo cha kuwa rais
Baada ya hoja hizo akahitimisha kwa kusema, kwa kuwa tayari tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imefuta uchaguzi, na kwa kuwa tayari tume hiyo imetangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi mkuu mwingine visiwani Zanzibar, na kwa kuwa hakuna mtu yeyote alieapa kiapo cha urais tofauti na rais wa sasa wa Zanzibar, Dkt Shein.
Hivyo Dkt Shein anatambulika kama rais wa Zanzibar na ana uhalali wote wa kuhudhuria katika uzinduzi wa Bunge la 11.

                

No comments: