![]() |
Marehemu Inspekta Gerald Ryoba na Gari iliyopata Ajali. |
Siku moja baada ya Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP),
Ernest Mangu, Inspekta Gerald Ryoba na familia yake kufariki dunia
kutokana na gari waliyokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika eneo la
Kongwa mkoani Dodoma, mashuhuda wa tukio hilo wamesimulia mwanzo mwisho
namna maafa yalivyowakuta.
Aidha, wakazi wa eneo hilo wameingiwa na hofu na kudai kuwa huenda kuna mzimu uliosababisha maafa hayo.
Maafa hayo yalitokea Jumapili Januari 3, 2016 majira ya saa tatu
usiku katika eneo hilo ambalo Inspekta Ryoba na familia yake akiwamo
mkewe Fidea John Kiondo, watoto wawili Gabriel Gerald Ryoba na Godwin
Gerald Ryoba, msichana wa kazi aliyefahamika kwa jina la Sara na dereva
wa gari hilo, F.3243 Koplo Ramadhan, wote walipoteza maisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mahojiano maalum na
Nipashe, wakazi hao walisema kila mwaka eneo hilo limekuwa likijaa maji
kutokana na uwapo wa mkondo wa maji unaotoka katika Kijiji cha
Hembahemba lakini hakujawahi kutokea maafa makubwa kiasi hicho
yaliyosababishwa na maji.
Inspekta Ryoba alipata ajali hiyo katika mtaa wa Majengo, Kibaigwa
wilayani hapa maarufu kwa jina la Bwawani alipokuwa akitokea Geita
kuelekea Dar es Salaam.
Akisimulia kuhusu maafa hayo, mmoja wa mashuhuda waliokuwapo katika
eneo hilo, ambaye ni mlinzi wa Kituo cha Mafuta (Sheli) cha Olympic
iliyopo jirani na eneo la tukio, Kinango Maganza, alisema hali hiyo
imewatia hofu kubwa kutokana na mvua iliyonyesha ilikuwa ni ndogo lakini
imesababisha maafa makubwa.
Alisema siku ya tukio mvua ilianza kunyesha majira ya saa 11:00
jioni na kukatika baada ya saa moja, lakini alishangazwa na kutokea kwa
wimbi kubwa la maji ambayo yalikuwa yakiingia katika barabara ya lami
kwa kasi na kufanya eneo hilo kujaa maji na magari kushindwa kupita.
Hata hivyo, alisema baadhi ya magari makubwa yaliendelea kupita kwa
mwendo mdogo lakini maji yalizidi kujaa na magari mengine ilibidi
yasimame.
“Mimi baada ya kuona magari yamesimama, niliingia ndani na
kuendelea na shughuli zangu, baadaye alikuja dereva wa Noah kugonga na
nilipofungua alikuwa akiomba hifadhi ya gari lake kutokana na kushindwa
kuvuka eneo hilo baada ya maji kuingia katika gari hilo na kulifanya
lizime na kushindwa kuwaka tena, hivyo walilifikisha sheli wakiwa
wanalisukuma,” alisema na kuongeza:
“Huyu dereva sina jina lake wala namba ya simu, yeye ndiye
aliyenisimulia hali halisi hadi hilo gari la huyo polisi liliposombwa na
maji kwa sababu alikuwa mbele yake wakiwa wanatazamana. Yeye alikuwa
akitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma na gari lililosombwa na maji
lilikuwa likitokea upande wa pili njia ya Dodoma kuelekea Dar es
Salaam,”alisema Maganza.
Maganza alisema kwa mujibu wa dereva huyo wa Noah gari hilo wakati
linavuka kulitokea wimbi kubwa la maji kutoka kushoto ambalo lilipiga
kioo cha mbele hali iliyomfanya dereva wa gari la Inspekta Ryoba
kushindwa kulimudu.
“Anasema wakati alipoona wimbi hilo yeye alizima gari na akabaki
pale pale alipo, sasa huyu aliyepata ajali yeye alianza kupita na
akakutana na hilo wimbi la maji na gari likateleza huku matairi mawili
yakiwa juu. Dereva huyo ndiye aliyetuambia ameliona gari limetumbukia
upande wa kushoto wa barabara,”alisema mlinzi huyo.
Alifafanua dereva wa Noah alikuwa akitokea barabara ya Dar es
Salaam-Dodoma na gari ya Inspekta Ryoba ilikuwa ikitokea barabara ya
Dodoma kwenda Dar es Salaam, na kwamba walikuwa mbele ya magari yote
yaliyokuwa yamesimama.
“Polisi walipata taarifa baada ya madereva wa mabasi yaliyosimama
kupiga simu na kuwajulisha kuwa kuna gari limesombwa na maji, hata
polisi wao walivyokuja ilibidi waje hapa kwenye kituo cha mafuta kukaa
hadi maji yalipopungua ndipo wakaanza jitihada za kulitafuta hilo gari,
huku wakizuia magari mengine yasipite,”alisema Maganza.
Alisema kwa upande wake, alishuhudia polisi wakitafuta gari hilo na
kutokana na wingi wa maji na tope zito ilifanya shughuli ya kulitoa iwe
ngumu na walipofanikiwa walikuta kuna maiti ndani ya gari hilo.
“Mimi nina miaka mitatu hapa, lakini sijawahi kushuhudia vifo vya
watu wengi kiasi hichi katika eneo hili ambalo kila mwaka maji hujaa
hasa msimu wa mvua na huwa hata siku moja hayavuki lami kuja upande
mwingine, hapa lazima kutakuwa na mizimu au jini,” alisema Maganza.
WAKAZI WA ENEO WASIMULIA
Naye mkazi wa eneo hilo, Leticia Ghamayu, alisema tangu aanze
kuishi katika eneo hilo hajawahi kusikia maafa makubwa kiasi hicho
ingawa baadhi husombwa lakini akadai huwa wanatoka hai.
“Haya maji huwa yanajaa hapa wakati wa msimu wa mvua lakini haya ya
juzi yaliyojaa hadi mawimbi makubwa kwa kweli kuna kitu jamani, hata
gari lenyewe sehemu iliyodondokea ni hatua tatu tu kutoka kwenye lami
lakini maiti zingine zimekutwa ng’ambo ya pili ya barabara,”alisema
mkazi huyo.
Alisema wakazi wa eneo hilo hukabiliana na hali hiyo kwa kutopita
hadi maji yapungue na magari husimama hadi maji yanapopungua ndipo
huendelea na safari.
“Hii barabara ya Dodoma- Dar es Salaam katika eneo hili la
Kibaigwa, mtanana na Pandambili sio bure kuna kitu maana licha ya haya
maafa hata ajali tu haziiishi ni mara kwa mara sasa sijui kuna jini au
mizimu,”alisema Ghamayu.
Alibainisha kuwa kwa sasa wananchi wameingiwa na hofu na hali hiyo
imekuwa gumzo kijijini hapo hivyo watakapoona hali hiyo wataacha kupita
hadi maji yaishe.
Hata hivyo, mkazi mwingine wa eneo hilo, Selemani Hamisi, alisema
tukio la kusombwa gari katika eneo hilo sio la kwanza kwani mwaka juzi
kuna gari ya wanajeshi ilisombwa lakini hakuna mtu aliyefariki.
“Mimi naona tatizo sio mizimu tu, itakuwa ni hili daraja ni dogo,
linashindwa kumudu maji hayo mengi yanayopita kutoka mkondo wa maji wa
Hembahemba hadi huko Kijiji cha Ndurugumi, yaani inabidi lijengwe daraja
kubwa ili roho zetu zisiwe juu juu,”alisema Hamisi.
Kwa upande wake, Helena Simba ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo,
alisema si mara ya kwanza eneo hilo kujaa maji, kwani zamani hali
ilikuwa mbaya zaidi na waliomba wawekewe daraja, lakini lilowekwa ni
dogo na halilingani na maji yanayopita katika eneo hilo.
“Kwa kweli hili eneo ni korofi, lakini halijawahi kuleta maafa
kiasi hichi, matukio ya watu kusombwa maji yapo lakini hakuna
aliyefariki, huwa wanaokolewa wakiwa hai, sasa hili la juzi limekuwa
gumzo mpaka watu wanahisi kuna jambo si bure,”alisema mkazi huyo.
Akizungumzia hali hiyo, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kibaigwa,
Fotina Wimbe, alisema vifo hivyo vya kusombwa na maji ni vya mara ya
kwanza kutokea katika eneo hilo ingawa kumekuwa na matukio ya watu
kusombwa na maji ila wakiokolewa wanakutwa hawajafa.
“Msongamano wa maji hapa ni wa muda mrefu, tatizo ni daraja dogo
maana hata mwaka juzi gari lilisombwa sijui lilikuwa la wanajeshi,
lakini hakuna aliyekufa ila safari hii hata hatuelewi hiki kitu gani
maana ni maafa makubwa…vifo vya watu nane,”alisema mjumbe huyo.
Aliongeza kuwa wamekuwa wakitambikia mizimu wakati wanapokosa mvua,
lakini kwa ajali mbalimbali zinazotokea katika eneo hilo hawajawahi
kutambika.
Alibainisha kwa tukio la ajali ya Inspekta huyo, wananchi wamekuwa
wakizungumza sana huku wakihusisha huenda eneo hilo kuna jini.
Mwili wa marehemu Inspekta Ryoba na familia yake ilisafirishwa jana
na kufika Kijijini kwao Kasamwa mkoani Geita majira ya mchana na maziko
yanatarajiwa kufanyika kijijini hapo leo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment