Friday, 8 January 2016

TBS WAAMURU PETROLI ILIYOINGIZWA NCHINI BILA VIWANGO SAHIHI IRUDISHWE UARABUNI.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeamuru shehena ya mafuta ya petroli iliyoagizwa kutoka Falme za Kiarabu irejeshwe ilikotoka kutokana na kubaini hayana ubora unaotakiwa kwa matumizi ya magari na mitambo.Akitoa taarifa hiyo Dar es Salam jana, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Joseph Masikitiko alisema, vipimo vya maabara vya sampuli ya mafuta hayo vimeonesha kuwa hayafai kwa matumizi.Alisema hayo ni matokeo ya ukaguzi wa hivi karibuni wa shehena hiyo yenye ujazo wa tani za metriki 38,521.018 katika meli ya MT. Ridgebury John B, yaliyokuwa yasambazwe na kuuzwa nchini.
Alisema, "Vipimo vinaonesha kuwa baadhi ya matakwa ya viwango vya mafuta ya petroli hayajafikiwa, hivyo kuamuru yarejeshwe yalikotoka. Kiwango cha ubora cha mafuta ya petroli ni TZS 672:2012/ EAS 158:2012 ambacho hakikufikiwa".
Matakwa ya kiwango ambacho mafuta hayo hayakukidhi ni pamoja na kuwa na kemikali zilizo na oksijeni ndani yake ambazo husababisha madhara kwenye injini za magari na mitambo.
Alisema, "Kiwango cha petroli hakiruhusu uwepo wa kemikali hizo kwenye mafuta hayo kwa sababu zinaua injini, kuhatarisha afya za watu na kuharibu mazingira kutokana na kusababisha moshi mchafu mwingi".

No comments: