Wasimamizi wa uwanja wa ndege Brazil wamezuia
takriban kilo 39 za siagi ya karameli kutoka timu ya mpira ya Uruguay
walipowasili kwa michezo ya kombe la dunia.
Siagi hiyo ilikamatwa kutoka kwa timu hiyo
ilipowasili katika uwanja wa ndege wa Confins karibu na kambi yao
wanakofanyia mazoezi,Sete Lagoas.Siagi hiyo inayojulikana kama ''dulce de leche'' ina umaarufu sana Uruguay lakini wasimamizi Brazil walisema kuwa kutengenezwa kwake kwa maziwa kunahitaji uhifadhi wa kiwango cha juu cha usafi ambao timu hiyo ya Uruguay haina uwezo wa kutimiza hilo.
Mashabiki wao tayari wameanza kulaumu utepetevu wa timu hiyo iliyocharazwa na Costa Rica mabao 3-1 kutokana na ukosefu wa siagi hiyo katika maankuli yao.
Msemaji kutoka kitengo cha kilimo cha Brazil aliiambia Reuters kuwa timu hiyo inaweza kurudishiwa siagi yao iwapo itapeana stakabadhi inayohitajika kuidhinisha kuingia nchini Brazil la sivyo watalazimika kusubiri hadi baada ya kukamilika kwa kampeni yao nchini humo .
Mlinda lango wa zamani wa timu hiyo Juan Castillo alisema kuwa timu hiyo ilibeba siagi hiyo walipoelekea Afrika Kusini mwaka wa 2010 na hawakuwa na tatizo lolote kutoka kwa wakuu nchini humo.
Dulce de leche inatengenezwa kwa maziwa,hamira na vanila na hutumiwa sana kwa kupakwa kwenye mkate,biskuti na kuchanganywa na matunda.


No comments:
Post a Comment