Thursday, 26 June 2014

Simba yafuata washambuliaji Brazil, Argentina

KUNDI la Friends of Simba limepania kuleta mabadiliko makubwa ndani ya klabu hiyo ili kuhakikisha inafanya vizuri katika michuano ya Ligi Kuu Bara msimu ujao, baada ya kutimkia nchini Brazil na Argentina kutafuta washambuliaji.
Uamuzi huo umefikiwa hivi karibuni katika kikao kilichowakutanisha wajumbe wa kundi hilo walipokuwa wakipitia majina ya wachezaji wanaotaka kuwasajili kwa ajili ya kuitumikia Simba kwenye michuano ya ligi kuu ili iweze kurudisha heshima yake iliyopotea kwa muda mrefu.
Hata hivyo, katika kikao hicho ndipo uamuzi huo ulipofikiwa, hivyo hivi karibuni baadhi ya viongozi wa Kamati ya Usajili ya Simba, watakwenda katika nchini hizo za Brazil na Argentina kwa lengo la kutafuta washambuliaji hao.
Mmoja wa wanachama wa Simba ambaye pia ni mjumbe wa kundi hilo la Friends of Simba, Azim Dewji, alisema kuwa wanataka kuleta mabadiliko makubwa katika timu hiyo ili kuwarudishia imani wapenzi na mashabiki wa timu hiyo ambayo waliipoteza kwa muda mrefu.
“Tumekuwa tukisajili wachezaji wengi kutoka katika nchi jirani lakini kumekuwa hakuna mabadiliko makubwa na ndipo nilipowashauri wenzagu na kuwataka angalau safari hii twende Brazil na Argentina kutafuta washambuliaji.
“Walikubaliana na wazo hilo na kuahidi kuwa watalifanyia kazi suala hilo, hivyo muda wowote kuanzia sasa baadhi ya wajumbe wa kamati yetu ya usajili watakwenda katika nchi hizo kwa lengo la kutafuta washambuliaji hao,” alisema Dewji.

No comments: