![]() |
Nabii T.B JOSHUA |
SERIKALI ya Afrika Kusini, imeshauriwa isitoe viza kwa nabii maarufu kutoka Nigeria, Temitope Balogun Joshua 'TB Joshua', kutokana na raia wake takriban 84 kupoteza maisha katika moja ya Ajali ya jengo la hosteli lililopo Synagogue Church of All Nations (Scoan), analolimiliki. "TB Joshua hawezi kuruhusiwa kuja Afrika Kusini hadi tufahamu kwa ufasaha namna ndugu zetu walivyopoteza maisha katika jengo lake," alisema Msemaji wa Umoja wa Vijana Chama cha ANC, Bandile Masuku wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya nchi hiyo. Kauli hiyo aliitoa juzi ikiwa ni siku chache baada ya TB Joshua kunukuliwa akisema atakwenda Afrika Kusini kutoa rambirambi zake kwa familia zote zilizokumbwa na mkasa huo ambao ni wa aina yake kwa kanisa analoongoza. "Tutahakikisha tunawasiliana na idara zote ili asipate viza," alisema Masuku. Watu zaidi ya 115 walipoteza maisha katika jengo hilo na wengine kadhaa kujeruhiwa. Inadaiwa kuwa takriban raia 350 wa Afrika Kusini walikuwa katika jengo lililoporomoka. Jumatatu, majeruhi 25 wa Afrika Kusini, wakiwemo watoto walipelekwa Pretoria kwa matibabu zaidi. Wakati hayo yakiendelea baadhi ya taarifa zinasema kuwa Serikali ya Afrika Kusini inataka TB Joshua alipe mamilioni ya fidia kwa waliopatwa na mkasa huo katika jengo lake. Wakati huo huo, Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria alitumia siku ya Jumamosi kutembelea eneo la tukio na kutoa pole kwa waliopoteza ndugu zao. Hata hivyo, hakupenda kuingia kwa undani zaidi kubainisha kuwa timu ya uchunguzi ndiyo itakayobaini ukweli. Pia, Nabii Joshua alinukuliwa akilalamika kuwa kuna hujuma katika suala hilo.
No comments:
Post a Comment