Sunday, 18 October 2015

MSAJILI WA VYAMA AONYA WANAOTAKA KUBAKI VITUONI.

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi
MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ameunga mkono kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa juzi katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Dodoma, ya kuwataka wananchi kurejea katika shughuli zao baada ya kupiga kura.

Aidha, amevitaka vyombo vya habari nchini kuhakikisha kuwa katika siku chache zilizobaki kabla ya Tanzania kufanya uchaguzi mkuu, vinahamasisha uchaguzi huo ufanyike kwa pande zote kuheshimu sheria na kuilinda amani ya nchi.
Jaji Mutungi aliyasema hayo Dar es Salaam juzi wakati alipokutana na waandishi wa habari waandamizi na wahariri kwa ajili ya kujadili hali ya kisiasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akifafanua suala la kuwataka wananchi kurejea katika shughuli zao baada ya kupiga kura, Jaji Mutungi alisema ni kweli sheria imeruhusu wananchi kubaki katika kituo cha kupiga kura kwa umbali wa mita 200, lakini sheria hiyo ina upungufu ambao wameuona ndio maana Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetoa kauli hiyo ya kuwezesha uchaguzi kufanyika katika mazingira ya amani.
Alihadharisha kwamba kama wapigakura wote wataamua kubaki katika vituo vya kupiga kura, hali hiyo itakuwa hatari na inaweza kutishia amani ya wananchi na kuogopesha wengine wanaotaka kwenda kupiga kura.
Kutokana na hali ya mivutano ya kisiasa, Jaji Mutungi alisema anatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari nchini katika kuihabarisha, kuelimisha na kusahihisha masuala yote yanayohitaji ama kukosolewa au kusahihishwa, ndio maana amewataka wanahabari kutumia kalamu zao kuwezesha uchaguzi wa amani.
“Najua nyie mnaaminika na chochote mnachoandika jamii inawaamini, hivyo nawaomba sana, mtumie nguvu yenu hii, kuyaanika yale yote mnayoona hayaendi sawa katika harakati hizi za uchaguzi, lakini pia naamini vyombo vyote nchini mkiweka msimamo kuwa mnataka uchaguzi uwe wa amani, hata hawa wanasiasa watafuata hivyo,” alisisitiza Jaji Mutungi.

No comments: