Tuesday, 1 December 2015

SERIKALI YA UINGEREZA YAIBUA KASHFA KUBWA YA TRILIONI 1.2/= KWA SERIKALI YA AWAMU YA NNE{TZ}.

Mh,Zitto Zuberi Kabwe.
SAKATA LINGINE LA TRILIONI 1.2/-
Serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la kuchunguza makosa ya jinai (AFO), imeibua kashfa ya rushwa katika ununuzi wa dhamana (hati fungani) ya serikali katika kipindi cha uongozi wa aliyekuwa Rais Jakaya Kikwete.
Madai hayo yametolewa jijini Dar es Salaam jana na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, katika taarifa yake aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari jana.
Katika taarifa yake hiyo, Zitto alidai kuwa biashara hiyo iliyofanyika kati mwaka 2011 na 2012, iliyohusisha serikali na benki ya Standard Group ya Afrika Kusini kupitia Stanbic ya Tanzania ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 600 (sawa Sh. Tanzania trioni 1.2).
Benki ya Standard Group ambayo ni benki mama ya Stanbic Tanzania, imekiri makosa hayo na kukubali kulipa faini ya Dola milioni 25.2 (sawa na Sh. bilioni 54 ) kwa kosa hilo.
Ilikubali kulipa faini hiyo mbele ya Jaji Lord Justice Leveson, wakati shauri hilo liliposikilizwa jana kwenye Mahakama ya Southwark nchini Uingereza.
Benki hiyo ilikubali shauri hilo limalizwe kwa njia ya muafaka baada ya kukiri ilitoa kiasi cha fedha ili kuwahonga maofisa wa Tanzania kinyume na Sheria ya Rushwa ya Uingereza ya mwaka 2010 kufanikisha mpango wao.
Pia benki hiyo imekubali kulipa kiasi cha Dola milioni saba (sawa na Sh. bilioni 15.1) kwa Serikali ya Tanzania kama fidia ya shauri hilo baada ya kubainika walihonga baadhi ya maofisa wa Tanzania kufanikisha mpango huo.
Hata hivyo, fedha hizo hazitakabidhiwa moja kwa moja kwa Serikali ya Tanzania bali zitapitishwa kwenye Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza ili kupangiwa kazi ya kufanya.

No comments: