Monday, 28 September 2015

TANZANIA KUPOKEA BIL 992 KWA AJILI YA KUTOKOMEZA SAKATA LA MGAO WA UMEME.

Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC walipokutana kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J. Hyde akiwa katika mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Jumamosi ya Septemba 26, 2015 New York nchini Marekani, wengine ni watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Kamran Khan,

Tanzania yaruka Vihunzi vya Rushwa na kupata Sh. bilioni 992.8 za Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC)

TANZANIA imetimiza masharti yote ya kupatiwa raundi ya pili ya fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia la Millennium Challenge Corporation (MCC) la nchini Marekani ambapo itaanza kupata na kunufaika na mabilioni hayo ya fedha kiasi cha Sh. bilioni 992.8 za kuboresha sekta ya umeme baada ya wajumbe wa Bodi ya MCC kupiga kura ya kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo chini ya Mpango wa MCC-2, FikraPevu imejulishwa. Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J. Hyde amemwambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Jumamosi ya Septemba 26, 2015 katika mkutano uliofanyika New York nchini Marekani na kuhudhuriwa na watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Kamran Khan, Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC ambapo Rais Kikwete yuko New York kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. "Hongera Rais Kikwete kwa sababu nchi yako, Tanzania imetimiza masharti yote ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC – 2, ikiwa ni pamoja na uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati kupambana na rushwa," Hyde amemwambia Rais Kikwete na viongozi wengine wa Tanzania akiwamo Waziri wa Nchi za Fedha wa Zanzibar, Yusuf Omar Mzee.
 Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu leo, imesema (FikraPevu imepata nakala) Hyde amemwambia Rais Kikwete kuwa Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17, mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, imeafiki kuhusu kipengele pekee kilichokuwa kimebakia katika masharti ya kupata fedha za MMC kutokana na Tanzania kukabiliana ipasavyo na rushwa na kuchukua hatua stahiki kukabiliana na janga hilo la rushwa. Aidha, MCC imetoa taarifa ya kuthibitisha kuwa Tanzania imetimiza masharti ya kuiwezesha kufaulu kupata raundi ya pili ya fedha za maendeleo na pia imetoa taarifa ya kuthibitisha kuwa ni kweli Bodi ya MCC imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na rushwa.
Tofauti na fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka igharimiwe na fedha hizo. Miongoni mwa wajumbe wengine wa Bodi ya MCC ni pamoja na Waziri wa Fedha wa Marekani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani duniani, Mwendeshaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), nafasi ambayo kwa sasa anaikaimu Bwana Alfonsi Lenhardt, Mtendaji Mkuu wa MCC Bi. Hyde na Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI) Balozi Mark Green. Mabalozi Lenhardt na Green walikuwa mabalozi wa Marekani katika Tanzania wakati wa majadiliano, upitishaji na utekelezaji wa MCC-1. Hyde, amesema sasa linalobakia ni kwa wajumbe wa Bodi kupelekewa muhtasari wa kuidhinisha mabilioni hayo kwa Tanzania ambayo chini ya mpango wa uwekezaji wa MCC-2 yatakwenda katika kuboresha huduma za umeme katika Tanzania ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme katika vijiji vingi zaidi nchini. Kiasi cha asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya asilimia hiyo imetokana na msaada wa MCC-1. Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC walipokutana kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Hata hivyo, chini ya Mpango huo wa pili wa MCC, Tanzania itapatiwa kiasi cha dola za Marekani milioni 472.8 (sawa na Sh. bilioni 992.80). Kwa kutilia maanani kiasi cha dola milioni 698 (sawa na Sh. trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini ya MCC-1 basi Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za Marekani trilioni 2.45 za maendeleo kutoka Marekani katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita.
Fedha za MCC-2 zitaanza kutolewa mwakani, 2016. Kiasi kilichotolewa kwa Tanzania wakati wa MCC-1 ndicho kilikuwa kiasi kikubwa zaidi ambacho kimepata kutolewa na Marekani chini ya Mpango huo wa Millennium Challenge Corporation na kwa kupita MCC-2 Tanzania itakuwa ni nchi ambayo itakuwa imepata kiasi kubwa cha fedha za maendeleo chini ya MCC duniani.
Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1 zilitumika kujenga Barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.
Aidha, fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara. Fedha hizo vile vile zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.

No comments: