![]() |
Mawakili wa serikali wakijadili jambo mara baada ya kuahirishwa kesi hiyo jana. |
![]() |
Waandishi wa habari wakifanya mahojiano na wakili wa serikali, Dk.Tulia Ackson mara baada ya kuahirishwa kesi hiyo katika Mahakama Kuu jana. |
![]() |
Wakili wa serikali Dk.Tulia Ackson akifanya mahojiano na wanahabari jana. |
![]() |
Wakili Peter Kibatala wa upande wa mlalamikaji akitoka katika chumba cha mahakama kwenye kesi hiyo hapo jana. |
JANA, mawakili wa serikali zaidi ya sita
wakiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa serikali, Dk.Tulia Ackson
walikuwa katika mvutano mkubwa na mawakili wa utetezi juu ya shauri la
tafsiri ya sheria ya Uchaguzi Mkuu unaotaka wapiga kura kukaa umbali wa
mita 200 baada ya kupiga kura, shauri lililoendelea katika Mahakama Kuu
jijini Dar es Salaam.
Majaji Sakieti Kihiyo, Aloysius Mjulizi
na Lugano Mwandambo, wa Mahakama Kuu, walitumia siku nzima kusikiliza
hoja za kisheria kuhusu shauri la katiba lililofunguliwa na Mgombea
Ubunge Viti Maalumu jimbo la Kilombero (Chadema), Amy Kibatala, akitaka
mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya kifungu cha 104 (1) cha sheria ya
Taifa ya Uchaguzi.
Mawakili kwa upande wa mlalamikaji
waliokuwa wakijibu hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo , ni Peter
Kibatala aliyeanza kutoa hoja zake kwa kuiomba Mahakama iangalie na
kutoa tamko kuhusu maana halisi na kusudio la kisheria la kifungu cha
104 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 kama wananchi baada
ya kupiga kura wanaruhusiwa kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200.
Katika hoja zake Kibatala alisema msingi
wa shauri hilo ni tamko la NEC lililotangazwa kwenye vyombo vya habari
kuwataka wananchi kukaa umbali wa mita 200 kutoka sehemu ya kupigia
kura.
Wakili wa serikali Dk.Tulia Ackson
alisema idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura ni 22,751292 kwa
Tanzania Bara hivyo kutokana na mwenendo wa siasa ambapo watu wamekuwa
na mwamko, idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na mazingira ya kupigia
kura na makazi ya watu kuweza kukaa kwa utulivu wakisubiri kumalizika
kwa kupiga kura. Hivyo kusisitiza maelekezo ya NEC kuwa sahihi.
Aidha Jaji Lugano alimtaka Dk.Ackson
kuisoma ibara ya 74 ya katiba ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania
kifungu cha 12 ambapo baada ya kusomwa, Jaji aliendelea kuwauliza
mawakili wa pande zote juu ya ibara hiyo.
Kesi hiyo inaendelea leo ambapo
inatarajiwa kuwa maelekezo maalum yatatolewa tayari kwa matumizi wakati
wa zoezi la kupiga kura keshokutwa Jumapili.
No comments:
Post a Comment