Tuesday, 10 November 2015

BUNGE WATOA UTARATIBU KWA WAGOMBEA NAFASI YA USPIKA.

Bunge la Tanzania.

Wakati Bunge la 11 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likitarajiwa kuanza vikao vyake Novemba 17, mwaka huu, kumekuwa na vita ya kimyakimya juu ya nani atakuwa Spika wa Bunge hilo.
Huku ikiwa tayari ofisi ya Bunge imeshatoa utaratibu ikisema majina ya wagombea yataanza kupokelewa siku mbili kabla ya Bunge kuanza, lakini hadi sasa hakuna chama kilichoweka wazi mchakato wake wa kuwapata waombaji wa nafasi hiyo na naibu wake.
Ofisi hiyo pia imeelekeza kuwa, mgombea ambaye si mwanachama wa chama cha siasa ambaye anataka kugombea nafasi ya Spika, anatakiwa kuwasilisha jina lake katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili kuthibitisha kuwa anasifa za kuwa Mbunge.
Mpaka sasa si CCM wala Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya Chadema, NCCR- Mageuzi, Cuf na NLD, hakuna kiongozi yeyote aliyezungumzia mchakato huo.
Hata hivyo, baadhi ya majina yanayotajwatajwa kinyemelea kugombea kiti hicho ni pamoja na aliyekuwa Spika wa Bunge la 10, Anna Makinda, aliyekuwa Naibu Spika, Job Ndugai pamoja na Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta.

No comments: